Moduli hii inajikita katika kuweka bayana maarifa ya jumla kuhusu fasihi na maarifa mahsusi kuhusu fasihi ya Kiswahili. Hivyo moduli inatalii maana ya fasihi, mitazamo kuhusu fasihi, asili ya fasihi, dhima za fasihi, na tanzu mbalimbali za fasihi na misingi ya uhakiki wa fasihi. Aidha, moduli inamtambulisha mwanafunzi katika kuitazama fasihi kama nyenzo ya ufundishaji wa lugha.
Moduli hii inazungumzia baadhi ya fasili za lugha, sifa za lugha, ufafanuzi wa dhana za isimu na historia yake fupi. Moduli hii pia inazingatia lugha na utamaduni, lugha kama mfumo. Zaidi ya hayo, moduli hii inazungumzia matawi ya isimu, viwango vya lugha, na inatoa muhtasari wa sifa za kisarufi ya Kiswahili kama vile vitenzi na nyakati za vitenzi, hali yakinishi na hali kanushi, aina za maneno, mnyambuliko wa maneno, vishazi na aina zake. Moduli hii pia inajadili muhtasari wa historia ya Kiswahili kwa kujadili asili yake, maendeleo na mchakato wa usanifishaji wake. Hatimaye, moduli inajadili dhana za fonetiki na fonolojia Hivyo basi, katika kazi za kivitendo, wanafunzi watafanya yafuatayo:
(i) Kufanya mjadala kuhusu kuhusu dhana muhimu za isimu ya Kiswahili kama vile matawi ya isimu, viwango vya lugha sifa za kisarufi na nyinginezo ;
(ii) Kufanya utafiti wa kina kuhusu mada mbalimbali zinazozungumziwa katika mihadhara au semina na kushirikisha matokeo ya utafiti wake kwa wenzake.