Moduli hii inaenda kwa anwani ya Uchambuzi wa Matini za Kifasihi na Uhakiki. Maneno makuu yanayojitokeza katika anwani hii sio mageni masikioni mwetu. Habib (2005) katika andiko lake lenye anwani ya “A History of Literary Criticism: From Plato to the Present” katika sehemu ya utangulizi anabainisha kwamba katika dunia yetu, imekuwa muhimu zaidi kuliko kipindi kingine chochote kujifunza kusoma kihakiki. Ijapokuwa yeye ameweka mkazo tu katika matini andishi. Ila kile anachokibainisha ni muhimu katika aina nyingine yoyote ya matini. Anazidi pia kusisitiza kuwa hatuwezi kuwa raia wema wawe ni wa nchi mahsusi au dunia kutokana na kujikuta tukiwa waathirika wa kani mbalimbali zinazotenda kazi duniani ambazo zinatuhamasisha kubakia tukiwa wajinga, kufuata kama vipofu iwe ni kwa jina la upofu wa kiutaifa, upofu wa kidini, au upofu wa uzalendo uliopitiliza. Anahitimisha kwa kutanabahisha kwamba, mojawapo ya funguo za kukabiliana na kani mbalimbali ambazo zingeweza kutuweka sisi katika uongo wenye giza ni desturi ya kujisomea ya mtu binafsi na taasisi yaani kujisomea kwa ukaribu, umakini na kihakiki.
Hivyo basi, Moduli hii imeandaliwa ili kutoa mwongozo na msaada wa ufundishaji uhakiki na uchambuzi wa matini katika kiwango cha juu. Inakusudiwa kukuza tathimini na ufurahiaji wa matini muhimu kwa upande wa wanafunzi. Moduli inaeleza bayana kwamba wanafunzi wanapaswa kujenga maarifa ya kichambuzi na kihakiki na pia kuwa na ufahamu matini wanazopewa kwa kuegemea katika uchambuzi wa kina wa matini hizo.
Moduli hii inahusu Mofosintaksia ya Kiswahili. Ni moduli inayozingatia vipengele mbalimbali vinavyohusiana na muundo wa Kiswahili kwa kuchunguza kwa pampja viwango vya Mofolojia na Sintaksia ya Kiswahili. Ili kuweza kutabiri maswala muhimu kuhusu Mofosintaksia ya Kiswahili, kiwango cha fonolojia nacho kimeshughulikiwa kwa kiasi fulani ili kutuwezesha kuyachanganua maswala muhimu ya Kimofolojia na yale ya Kisintaksia. Hivyo basi, dhana muhimu zinazoambatana na Fonolojia, Mofolojia na Sintaksia zitatiliwa mkazo ambapo muundo wa lugha ya Kiswahili utachanganuliwa kwa jumla huku tukizingatia nadharia za kisasa za isimu.