Moduli hii inatarajiwa kumfanya mwanafunzi afahamikiwe ujuzi wa jumla kuhusiana na fasihi linganishi kwa ajili ya lugha katika elimu. Wanafunzi watatambulishwa kwa masuala mengi mtambuka ya kinadharia, matini za kifasihi, kutalii masuala ya kihistoria na sasa yanayohusiana na usasa, usasaleo na utanadawazi. Hii itawasaidia wanafunzi kuchambua kazi mbalimbali za kifasihi kutoka katika visasili, dhamira na motifu za kiutu na zile za mikabala ya kifeministi zinazojitokeza kati sio tu katika tamaduni na nyakati tofauti bali pia zinajitokeza kwa waandishi tofauti pamoja na tanzu tofauti. Haya yote yatatazamwa mkazo ukiwekwa katika malengo ya ufundishaji wa lugha na fasihi katika elimu. Hii ikiwa na maana ya ufundishaji wa fasihi linganishi kwa minajili ya kufundishia lugha na fasihi katika elimu.
Moduli hii inalenga kumpa mwanafunzi uwezo wa kufanya uchunguzi wa kina katika semantiki, leksikolojia, teminolojia na pragmatiki katika muktadha wa elimu. Moduli hii inatarajia pia kumwezesha mwanafunzi kupata stadi za kufanya utafiti na uhakiki wa tafiti za hivi karibuni katika nyanja za semantiki, leksikolojia, teminolojia na pragmatiki kwa ajili ya matumizi yake katika elimu. Hatimaye, mwanafunzi ataweza kufanya kazi mbalimbali kwa kueleza na kuhakiki tafiti zilizojitokeza katika utunzi wa kamusi na pragmatiki katika Kiswahili na hata kuchunguza msamiati na kamusi mbalimbali zilizoandikwa katika lugha ya Kiswahili.
Moduli hii ni inahusu Uchakataji wa lugha na utumizi katika Kiswahili. Ni moduli inayozingatia vipengele mbalimbali vinavyohusiana na maswala ya lugha kwa kuchunguza hali na mbinu za menejimenti ya lugha, uhusiano kati ya lugha na akili pamoja na mchakato wa lugha unaoathiri ujifunzji na ufundishaji wake. Aidha, moduli hii inalenga kumwezesha mwanafunzi kushiriki katika mijadala mbalimbali kuhusu Menejimenti ya lugha, na matumizi ya lugha katika elimu. Vilevile, moduli hii itamwezesha pia kupendekeza masuluhisho kwa masuala mengi yanayohusiana na upangaji lugha kwa kuchunguza uhusiano uliopo kati ya lugha na fikra, na lugha na Tekinolojia ya kisasa ambapo nafasi yake katika ujifunzaji na ufundishaji wa lugha itachunguzwa. Hivyo, Moduli hii itazingatia vipengele muhimu vifuatavyo : Upataji na ujifunzaji lugha Upangaji lugha, Lugha na fikra pamoja na Isimu Kokotozi.